Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mkurugenzi wa bodi ya shirika la kupambana na ulanguzi wa mihadarati na vileo nchini Nacada Sheikh Juma Ngao amesema kwamba idara ya usalama na mahakama zinachangia kuenea kwa mihadarati eneo la Pwani, na akazitaka kuwazuilia walanguzi wa mihadarati wanapotiwa nguvuni ili kusaidia kwa uchunguzi.

Akizungumza mjini Mommbasa siku ya Jumatatu, Sheikh Ngao amesema kwamba kuzuiliwa kwa walanguzi wadogo na watumizi wa dawa za kulevya eneo la pwani kamwe hakutasaidia kusitisha kuenea kwa mihadarati, na akasema kwamba lazima kwa idara hiyo kuzidisha juhudi zao na kuwakamata walanguzi wakuu.

Sheikh Ngao amesema kwamba hatua ya idara ya mahakamani kuwaachiliwa kwa dhamana kwa washukiwa wa dawa za kulevya wanapofikishwa mahamani kunachangia kuwepo kwa changamoto za kukabiliana na walanguzi wa mihadarati humu nchini, kwani hatua hiyo inazidisha kuwapa nafasi ya kuendeleza bishara hiyo haramu.

Wakati uo huo, amewashinikiza viongozi wa kisiasa kutokwepa majukumu yao ya kupiga vita utumizi wa miahadarati na vileo katika eneo la Pwani, na akasema kwamba iwapo viongozi hao watajitolea kikamilifu, basi kwa kiwango kikubwa biashara hiyo itasitishwa.

"Tuko na changamoto kubwa ya kukabiliana na watumizi wa mihadarati, na iwapo idara ya polisi na mahakama zitashirikiana, basi janga hilo litakabiliwa na wanasiasa, lazima wajitokeze kupiga vita mihadarati ili kutuwezesha kufaulu kulikabili janga hili," alisema Ngao. 

Mkurugenzi huyo wa bodi ya shirika hilo ameahidi kuzuru mashinani na kuendeleza hamasa kwa jamii kufahamu jinsi ya kujitenga na utumizi wa dawa za kulevya na vileo nchini.