Share news tips with us here at Hivisasa

Bodi ya utalii nchini imeihimiza idara ya usalama kuhakikisha kuwa usalama unaimarishwa zaidi katika maeneo ya bahari hindi, ardhini na angani ili kuzuia sekta ya utalii kutokumbana na changamoto.

Katibu wa bodi hiyo Allan Njoroge amesema kuwa kutekwa nyara meli katika maeneo ya bahari hindi kunachangia zaidi kusitishwa kwa meli za kitalii kuzuru humu nchini.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Njoroge alisema kwamba iwapo swala hilo litachukuliwa kwa makini, basi sekta ya utalii itaimarika na mageni na watalii watazuru kwa wingi hususana eneo la Pwani, japo akasema kwamba bodi hiyo imeweka mikakati mwafaka ya kukabiliana na changamoto zilizopo.

“Ni lazima kwa serikali kupitia idara ya usalama kuimarisha zaidi usalama katika maeneo ya bahari hindi na angani ili kuona kwa sekta ya utalii inalindwa vyema,” alisema Njoroge.

Afisa huyo aidha amewahimiza wadau mbalimbali katika sekta ya utalii kuhakikisha kuwa wanashirikiana na bodi hiyo pamoja na wizara ya utalii nchini ili kukabiliana na changamoto zinazoikumba sekta hiyo na kuiboresha zaidi.

“Tunawashauri pia wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kuhakikisha kuwa wanashirikiana na bodi yetu pamoja na wizara ya serikali kuhakikisha kuwa sekta yetu tunainua zaidi,” aliongeza Njoroge.

Wakati uo huo, Njoroge amesema kuwa bodi hiyo inatarajia kupokea meli tatu za kitalii kabla mwishoni mwa mwezi Februari mwaka ujao, hatua ambayo itapiga jeki kwa kiwango kikubwa sekta hiyo.