Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya masuala ya vijana na jinsia kwenye Kaunti ya Nyamira imeshtumiwa kwa kutojihusisha kikamilifu na masuala ya vijana wa Borabu, ili kuwasaidia kuimarisha maisha yao.

Akihutubu kule Borabu siku ya Jumapili, alipokuwa akisimamia fainali ya mechi ya kuwania kikombe cha Getena, mwanasiasa Nyandoro Kambi alisema kuwa idara ya vijana haijafanya juhudi ili kuimarisha maisha ya vijana katika eneo hilo.

"Msimamo wangu kuhusiana na idara ya masuala ya vijana huku Nyamira bado ungali ule ule kwasababu sijaona lolote zuri likijitokeza kutoka kwa idara hiyo. Vijana wanaendelea kuhangaika na hali ya umaskini licha ya kuwepo kwa idara inayofaa kushughulikia maslahi yao,” alisema Kambi.

Kwa upande mwingine, Kambi aliisihi idara hiyo ya vijana kuhakikisha kuwa imeweka mikakati ili kuimarisha maisha ya vijana katika eneo hilo.

“Ni jambo la kutia moyo kujua kuwa vijana wengi wanaendelea kujihusisha na biashara. Yafaa idara ya masuala ya vijana na jinsia iweke mikakati kabambe ili kuhakikisha vijana wanapata ufadhili wa kifedha ili kujistawisha,” alisema Kambi.