Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imewahakikishia wakaazi kuwa shughuli ya upigaji kura wa uchaguzi mdogo wa Malindi utafanyika vyema.

Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari siku ya Jumapili, Kamishna wa tume hiyo Yusuf Nzibo alisema kuwa maafisa wa tume hiyo walijiandaa vyema kusimamia shughuli hiyo, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huo ni wa huru na haki.

Nzibo alisema kuwa tume hiyo haiegemei upande wowote wa kisiasa bali uamuzi utakaotolewa ni ule wakaazi watakao kuwa wameamua kwenye shughuli hiyo ya upigaji kura, na kuongeza kuwa uchaguzi huo utakuwa wa wazi.

“Tungependa kuwahakikishia wakaazi wa Malindi kuwa shughuli ya upigaji kura wa eneo bunge hili utakuwa wa huru na haki na wala maafisa wa Tume ya IEBC hawataegemea upande wowote wa kisiasa. Tume yetu ni huru hivyo basi wakaazi wajitokeze kwa uchaguzi huo,” alisema Nzibo.

Wakati huo huo, aliwahakikishia wakaazi kuimarishwa kwa usalama wakati wa shughuli hiyo na kusema kuwa maafisa wa usalama watakuwa katika kila kituo katika eneo bunge hilo, licha ya kuwa na vituo zaidi ya 50.

Uchaguzi huo utafanyika siku ya Jumatatu kwa minajili ya kuziba nafasi ya Dan Kazungu, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Madini nchini.