Huenda zoezi la usajili wa wapiga kura katika eneo la Pwani likakumbwa na changamoto iwapo makamishna wa tume huru ya Uchaguzi na mipaka nchini IEBC watakosa kuwafikia wakazi wa mashinani kuwahamisha kuhusu umuhimu wa usajili huo.
Kulingana na kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa Maxwell Masai, idadi kubwa ya vijana na akina mama katika eneo hilo bado hawajafahamu umhimu wa usajili huo, wakisema kuwa wengi wao hawana vitambulisho vya kitaifa.
Akizungumza katika mkutano wa vijana huko Kisauni mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Masai alisema kuwa kuna haja ya makamishna wa tume hiyo kuzuru mashinani na kuwaelimisha vijana na akina mama pamoja na kuwahimizwa kuchukua vitambulisho vya kitaifa ili kuhusishwa katika usajili wa wapiga kura.
“Tunaiomba tume ya IEBC kuhakikisha kuwa makamishna wake wanafika hadi mashinani kuwahamisisha wakazi kuhusu umhimu wa usajili wa wapiga kura ili kufikia malengo yake ya kupata zaidi ya watu milioni 14 kama inavyotarajia kwa sababu wengi wa wakaazi hawana ufahamu,” alisema Masai.
Masai aidha amewataka wakazi wa kaunti hiyo na eneo zima la Pwani kujitokeza kwa wingi kujisajili kama wapiga kura ili kuwachagua viongozi waadilifu na wawajibikaji katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Mapendekezo ya kiongozi huyo wa vijana yanajiri huku zikisalia siku nne kabla ya zoezi hilo la usajili wa wapiga kura kuong’onanga rasmi tarehe 15 mwei Februari mwaka huu.