Mwakilishi wa wadi ya Gesima ameitaka Tume ya IEBC kuhakikisha kuwa watu wakongwe na hata pia wanaoishi na ulemavu wanapata fursa ya kujisajili kama wapiga kura.
Akihutubu katika eneo la Gesima siku ya Jumatatu, Ken Atuti alisema tume hiyo haijaweka bayana jinsi ambavyo itakavyoweka mikakati ya kuwafikia watu wanaoishi na ulemavu na wakongwe, ili nao wajisajili kama wapiga kura.
"Ninajua kwamba tuna wazee na hata pia watu wanaoishi na ulemavu wa aina mbalimbali ambao kwa kweli hawawezi kutembea kwa muda mrefu ili kufika katika vituo vya kujisajili kama wapiga kura. Tume ya IEBC haijaeleza bayana jinsi watu wa aina hii watakavyo jisajili," alisema Atuti.
Atuti aidha aliipa changamoto tume hiyo kuhakikisha inaajiri angalau karani mmoja katika kila eneo la uwakilishi wadi, ili makarani hao wawe wakitembea na kusajili watu wa aina hiyo vijijini.
Alisema kuwa hatua hiyo itawawezesha watu wanaoishi na ulemavu na wazee kupiga kura kwa maana hiyo ni haki yao.
"Sidhani kwamba tume ya IEBC imeweka mikakati ya kutosha ili kuajiri makarani wa kutosha watakaoendesha shughuli ya kusajili wapiga kura vijijini. Ingekuwa bora iwapo watu wasio na uwezo wa kusafiri hadi kwenye vituo watapewa nafasi ya kujisajili wakiwa nyumbani," aliongezea Atuti.