Kuna haja ya kuwekwa mikakati madhubuti ili kuona kuwa utaratibu wa kupiga kura unaanza na kuendelea ili kumfikia kila Mkenya ambaye amefikisha umri wa kujiandikisha kupiga kura.
Haya ni kwa mujibu wa mbunge wa eneo bunge la Jomvu Badi Twalib, ambaye ameendeleza shutuma dhidi ya Tume ya IEBC.
Mbunge huyo alidai kuwa tume hiyo imekuwa ikiwafeli Wakenya kwa kukosa kuwa na mipangilio imara ya kuhakikisha kuwa Wakenya wote wanaandikishwa na kupata haki za kupiga kura.
Akiongea siku ya Jumatatu katika eneo bunge lake, la Jomvu, Twalib aliwataka vijana wote ambao wamefikisha umri wa kupiga kura kuhakikisha kuwa wanajiandikisha wakati huu ili kuepuka kukosa kushiriki na kupigia kura viongozi wanaowapenda kufika mwaka wa uchaguzi mkuu ujao.
Shughuli ya kuwaandikisha wapiga kura ilianza siku ya Jumatatu na inatarajiwa kuendelea kwa muda wa mwezi mmoja ambapo tume ya uchaguzi IEBC inalenga kuwasajili zaidi ya wakenya milioni nne, ambao wamefikisha umri wa kupiga kura kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa 2017.
Hata hivyo, tayari viongozi wa upinzani wakiongozwa na kinara wa muungano wa CORD Raila Odinga wametoa tetesi kuwa serikali ya muungano wa Jubilee inapendelea sehemu zinazoaminika kuwa na wafuasi wengi wa chama hicho.