Seneta wa Mombasa Hassan Sarai ameishutumu tume huru na mipaka IEBC kwa kusajili wapiga kura wachache kwenye ngome za upinzani kinyume na sehemu zinazounga mkono serikali.
Akizungumza siku ya Jumapili katika ukumbi wa Little Theartre jijini Mombasa, katibu mkuu wa chama hicho Omar ameitaka tume hiyo kuongeza vifaa vya uwandikishaji wapiga kura katika wadi zote nchini kutoka kifaa kimoja kwa kila wadi hadi kifaa kimoja kwa kila kituo cha upigaji kura.
Kauli hii inajiri huku zoezi la usajili wa wapiga kura likitarajiwa kuanza mwezi ujao kote nchini.
Haya yanajiri baada ya tume hiyo kutangaza kuwa itawasilisha mitambo yao katika kituo kimoja pekee kila wadi kote nchini.
Wakati huo huo, mwanasiasa Ali Mbogo alisema kuwa huenda idadi kubwa ya watu wakakosa kujiandikisha kama wapiga kura nchini kutokana na hatua hiyo ya IEBC, iwapo ni kituo kimoja pekee kitachotumika kujiandikisha katika kila wadi.
Mbogo ametoa wito kwa tume hiyo kujitahidi kusambaza mitambo hiyo katika kila kituo cha upigaji kura ili wananchi wajiandikishe kwa wingi na kushiriki haki yao ya kidemokrasia.
Zoezi hilo la usajili wa wapiga kura linatarajiwa kufanyika kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Februari 15 hadi Machi 15 mwaka huu ambapo tume hiyo inalenga kusajili wapiga kura million 22.4 kote nchini.