Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC imezindua rasmi zoezi la kuwasajili wapiga kura huku ikilenga kuwasajili takriban wapiga kura milioni 4 kwa muda wa mwezi mmoja ujao.

Akiongoza shughuli hiyo iliyoandaliwa katika ukumbi wa Pumwani, Nairobi,mwenyekiti wa tume hiyo, Isaak Hassan, kwa mara nyingine tena amewasihi Wakenya walio na vitambulisho vya kitaifa kujitokeza kwa wingi ili kujisajili kwani ndio njia ya kipekee ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Gavana Evans Kidero alisema kuwa wanatarajia zaidi ya wapiga kura 500,000 kutoka kaunti ya Nairobi.

Kwenye shughuli hiyo, tume hiyo imesema inapania kutumia mitambo 5,756 ya BVR kwenye wadi zote 1,450 huku kukiwa na wataalamu 290 wanaoendelea kupokea mafunzo ili kuwawezesha kushughulikia kasoro zozote za kimitambo. Aidha, tume hiyo imesema itakuwa na jumla ya vituo 24,559 vya kuwasajili wapiga kura.

Tume hiyo aidha imekanusha madai ya mrengo wa upinzani kuwa tume ya IEBC inapendelea ngome za muungano wa Jubilee kwa kuzitengea vifaa vingi zaidi ikilinganishwa na ngome za muungano wa CORD.

Shughuli hiyo ya usajili itaendelezwa hadi tarehe 15 Machi, 2016.