Hatua ya serikali kuwafuta kazi wakuu wa Shirika la Huduma za Feri inazidi kuibua hisia kinzani kutoka kwa Wakenya mbali mbali, wadau wa sekta ya utalii na uchukuzi nchini.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, afisa mtendaji wa muungano wa wahudumu wa hoteli na wapishi mkoani Pwani, Sam Ikwaye, alisema kuwafuta kazi wakuu hao hakutaleta suluhu ya kudumu kwa changamoto ambazo zimekuwa zikiwakumba wasafiri wanaotegea huduma za Feri.
Badale yake, Ikwaye, amehimiza serikali kujenga daraja itakayounganisha kisiwa cha Mombasa na Pwani Kusini, ili kuimarisha shughuli za uchukuzi na kupunguza misongamano ya mara kwa mara inayoshuhudiwa katika kivuko hicho, hasa nyakati za asubuhi na jioni.
Afisa huyo vile vile aliilaumu serikali kwa kutotoa ufadhili wa kutosha kwa Shirika la Feri, huku ikishinda ikitaka huduma bora na kutishia kuwafuta kazi wakuu wake kwa madai ya kutowajibika.
“Wanaotegemea huduma za feri wanazidi kuongezeka kila siku lakini serikali haiongeza pesa kwa usimamizi. Huduma bora utapatikanaje?” aliuliza Ikwaye.
Inadaiwa wenye hoteli wengi walilazimika kutumia ndege kuwasafirisha watalii kutoka Mombasa hadi Diani na Kwale, msimu wa Krismasi na mwaka mpya kufuatia msongamano mkubwa ulioshuhudiwa katika kivuko cha Feri Likoni.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama cha utalii tawi la Pwani, Mohammed Hersi, ameipongeza hatua ya serikali huku akisema mabadiliko yalihitaji na hata yamekuja kuchelewa.
Hata hivyo, amehimiza serikali kumregesha kazini aliyekuwa mkuregenzi wa huduma za Feri Alex Leteipan huku akimtaja kama mtu wa pekee anayeweza kuleta mabadiliko katika kivuko hicho.
“Leteipan alifanya kazi nzuri alipokuwa madarakani, huduma zake zilipendeza. Itakuwa jambo la busara kwa serikali kumregesha tena,” alisema Hersi.
Siku ya Jumatano, serikali ilimfuta kazi mkurugenzi wa huduma za Feri Musa Hassan Musa, mhandisi mkuu George Nyando na meneja wa operesheni Anthony Muzungu saa 48 baada ya Rais Kenyatta kufanya ziara ya ghafla katika kivuko hicho.