Share news tips with us here at Hivisasa

Uamuzi kuhusiana na kesi ambapo mwanamme mmoja anadaiwa kumuuwa babake unatarajiwa kutolewa mwezi Machi mwaka huu na mahakama moja ya Nakuru.

Mshtakiwa huyo kwa jina la Clement Muchoki anadaiwa kumuuwa babake Issac Kagwamba kwa kumgonga kwa kipande cha chuma kichwani mwaka wa 2013 mwezi Februari tarehe 3 katika kijiji cha Gitura, eneo la kabazi lililo mjini Subukia katika kaunti ya Nakuru, shtaka ambalo tayari amelikanusha.

Alhamisi tarehe 28 Januari, kakake Muchoki anayefahamika kama David Muriithi aliyetoa ushahidi wake mbele ya jaji Maureen Odero alieleza mahakama kwamba hakufahamu kuhusiana na mzozo wowote ambao ungepelekea kakake kusababisha kifo cha babake.

Kwa upande wake, daktari kwa jina la Daniel Wainaina aliyewasilisha ushahidi wake mahakamani alikariri kwamba kulingana na uchunguzi wake, marehemu alikuwa na majeraha yaliyosababishwa na kifaa cha chuma kichwani, akiongeza kwamba kifo chake kilitokana na damu iliyofuja kutoka kichwani mwake kutokana na jeraha lililosababishwa na kifaa hicho.

Kulingana na jaji Odero, uamuzi kuhusiana na kesi hiyo utatolewa mwezi Machi tarehe 23 mwaka huu.