Kulitokea hali ya hati hati baada ya mwanamume mmoja kuanguka katika Bahari Hindi siku kuu ya Krismasi kutoka kwenye feri alimokuwa ameabiri katika kivuko cha feri cha Likoni katika Kaunti ya Mombasa.
Mtu huyo ambaye inasemekana alikuwa ameabiri feri kutoka eneo la Likoni na kuelekea kisiwani Mombasa, alikuwa amekaa katika upande mmoja wa lango kuu la kuingia magari na watu kwenye feri ambapo alishtukia ameanguka majini.
Kulingana na mama Halima Swale, ambaye alikuwa katika feri hiyo husika, ni mwanaume huyo ambaye hakufahamika kwa majina alikuwa amesima upande wa nyuma langoni, ambapo aliteleza na kuingia baharini baada ya feri kung’oa nanga kuelekea upande mwingine wa kuegesha kisiwani Mombasa.
“Mimi nilikuwa upande wa juu wa feri nikaona mtu anaanguka kwenye bahari na kuanza kujiokoa kwa kupiga mbizi ambapo mwendesha feri alifanya juhudi kumuokoa lakini hakuweza,” alisema Swale.
Ilichukua juhudi za mwendesha feri kuwaita polisi wa bandarini kuja na mashua yao na kumwokoa mwanaume huyo na kupelekwa ili kufanyiwa huduma ya kwanza.
Hata hivyo, walioshuhudia kisa hicho walidai kuwa mwathiriwa alikuwa ameonja kinywaji na ni yeye alijaribu kujirusha kwenye bahari kwani alitoka upande wa juu na kutaka kupishwa.
Waliongeza kuwa hakuonyesha dalili yoyote ila walishtukia mtu akiwa majini kwa vile alikuwa amesimama mwisho, na tayari feri ilikuwa imebeba watu wengi ambao walikua wanatoka sehemu mbali mbali kutoka sherehe za krismasi.