Share news tips with us here at Hivisasa

Jamii ya Isahakia inayoishi mjini Naivasha sasa imeitaka tume ya ardhi nchini kukoma kuingilia maswala ya ardhi ambayo ina kesi mahakamani.

Jamii hiyo imesema kuwa imegadhabishwa na semi za mwenyekiti wa tume hiyo Mohamed Swazuri kuhusiana na kipande kimoja cha ardhi kilichoko mjini Naivasha na ambacho utata wake kuhusiana na umiliki umo mahakamani.

Kulingana na mwenyekiti huyo, utata unaozingira ardhi ya shirika la utafiti wa maswala ya Kilimo (KALRO) na wao imo mahakamani, na tume hiyo ilifaa kuiacha mahakama kuitatua.

Kwenye kikao na wanahabari mapema Jumanne, mwenyekiti wa jamii hiyo Ali Farah alisema kuwa swala hilo limekuwa kwenye mahakama kuu ya Nakuru kwa zaidi ya miaka miwili.

“Jamii hii ina matumaini ya kupata ardhi hii tulioachiwa na mababu zetu kupitia kwa mahakama na wala si kwa tume hiyo ya Swazuri,” alisema Farah.

Awali jaji wa mahakama kuu Silas Munyao alikuwa amepuuzilia mbali ombi la kutaka kesi hiyo ihamishwe hadi mjini Nairobi kutoka Nakuru, huku pia akipuuzilia mbali ombi la KALRO la kumtaka kujiuzulu kusikiza kesi hiyo.