Jamii ya wafugaji inayoishi mjini Naivasha siku ya Jumatatu iliteta vikali hatua ya kutopewa vitambulisho kwa vijana wao katika eneo hilo.
Jamii hiyo aidha imelaumu idara ya utawala wa mikoa kwa kuleta mzozo uliopo kwa sasa, huku wakisema kuwa wamekosa kazi kutokana na ukosefu wa vitambulisho.
Haya yaliibuka wakati wa kukutana kwa baraza hilo katika shule ya msingi ya Namucha katika wadi ya Mai Mahiu, ambapo waliisuta serikali kwa kukosa kuwajibika.
“Baadhi ya vijana wetu wamekuwa wakisubiri vitambulisho kwa zaidi ya miaka miwili sasa,” mwenyekiti wa jamii hiyo Joseph Ole Kishau alisema.
Kishau aidha alisema kuwa juhudi za kutafuta usaidizi kutoka kwa serikali kuu zimekuwa zikigonga mwamba kila wakati wanapotaka kujibiwa.
Naye pasta Lorna Longushu alisema kuwa wamekuwa wakitengwa kwenye nyadhifa zote za uongozi kwa kukosa vitambulisho na sasa hawajui watakoenda.
Mkuu wa wilaya hiyo Abraham Kemboi, ambaye alihudhuria mkutano huo alisema kuwa atachukua swala hilo kwa idara husika ili vitambulisho hivyo vichukuliwe.