Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku zoezi la usajili wa wapiga kura likiendelea kote nchini, jamii ya watu wanaoishi na ulemavu wamehimizwa kujisajili ili waweze kuwachagua viongozi watakaotekeleza maswala yao.

Mwakilishi wa walemavu katika bunge la kaunti ya Mombasa Hudson Kalume amesema kuwa jamii ya walemavu inafaa kujihusisha kikamilifu katika zoezi hilo ili waweze kuchagua viongozi watakao wawakilisha kikamilifu serikalini na kuwabandua wale wabinafsi.

Kalume ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ‘fursa sawa kwa wote’ katika bunge hilo, ameeleza kuwa kujisajili kwa walemavu kutawapa fursa ya kutambulika na jamii huku amehimiza kujitosa katika ulingo wa kisiasa kwani wana haki kikatiba.

“Tunawaomba walemavu kujitokeza na kujisajili kwa wingi kama wapiga kura ili kuwabandua viongozi wasiojali maslahi ya walemavu na kuwachagua viongozi bora ili kuleta mabadiliko kwa walemavu,” alisema Kalumu mjini Mombasa kwenye mkutano na wanahabari siku ya Jumatatu.

Kiongozi huyo ameihakikishia jamii ya walemavu kuwa maswala yao yatazingatiwa iwapo watajihusisha kikamilifu katika upigaji kura wakati utakapowadia.