Huku jamii ya waislamu na waumini wa dini hiyo kwa jumla wakisherehekea siku kuu ya Maulidi, wakenya wote wametakiwa kushikana mikono na kupiga vita uhalifu na ugaidi miongoni mwa vijana kote nchini.
Akiongea akiongea na waandishi wa habari baada ya sherehe hizo siku ya Jumapili kwenye mtaa wa Kisauni, jijini Mombasa, Athman Saidi ambaye ni mkereketwa wa vita dhidi ya ugaidi na mshauri wa vijana alisema kuwa wakati umefika kila mzazi pamoja na jamii kwa jumla kuja pamoja na kuepusha vijana dhidi ya kujiunga na makundi haramu ambayo yamekuwa yakiwahangaisha wakenya kwa muda mrefu.
Athman alidokeza kuwa yeye na makundi mengine na mashirika ya kijamii watashirikiana ili kuhakikisha kuwa ujumbe wa amani unawafikia vijana ambao ndio wamekuwa wakilengwa na makundi ya kigaidi kwa kupewa mafunzo ya itikadi kali na kutumiwa kuuwa watu wengine.
“Sharti tuje kama jamii moja kwenye mkondo mmoja wa kushirikiana kwa kupiga vita ugaidi na itkadi kali miongoni mwa jamii, hasa vijana wetu ambao wamekuwa wakipotea na kutumiwa vibaya na makundi kama Al Shabaab, sisi kama wazazi tuna jukumu la kuwaongoza wana wetu kwa njia ifaayo,” alisema Athman.
Amesema haya huku vikosi vya wanajeshi wa KDF wakiendelea kupigana na magaidi ambao wanaaminika wamejificha katika msitu wa Boni, ambapo serikali imetangaza kuwa itapigana hadi mwisho.