Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Afisa wa maswala ya watoto katika Shirika la Utetezi wa haki za kibinadamu la Muhuri, Topister Juma amesema kuwa kaunti ya Mombasa imeripotiwa kuwa na idadi kubwa ya visa vya ubakaji kutokana na kuzembea kwa baadhi ya wazazi. 

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumma, afisa huyo alisema kuna haja ya jamii kujitokeza waziwazi na kupinga dhulma za kijinsia ikiwemo ubakaji ili kuona kwamba mtoto wa kike inalindwa vyema dhidi ya visa hivyo.

Topister amesema kuwa Idara ya mahakama na maafisa wa serikali wanaohusika na mambo ya jinsia wanafaa kubuni sheria kali dhidi ya wanaotekeleza ubakaji ili kupata suluhu la kusitisha uovu huo katika kaunti ya Mombasa na kwengine eneo la Pwani.

"Kaunti ya Mombasa imeripotiwa kukithiri kwa dhulma za kijinsia ikiwemo ubakaji kwa kiwango kikubwa na hakuna hatua zozote zimechukuliwa kuwalinda watoto hawa wadogo wa kike, basi sisi tunataka kuona kwamba haki inatendewa watoto hawa na sheria kali ziidhinishwe dhidi ya wahusika," alisema Topister.

Amesema kuwa hatua ya kisa cha hivi maajuzi cha kutoroshwa kwa mtoto wa umri wa miaka 12 na kisha kubakwa na kupachikwa mimba ni ukiukaji mkubwa wa haki za watoto na lazima wahusika kuadhibiwa kisheria.

Mwanaharakati huyo wa kijamii ameahidi kuishinikiza serikali pamoja na idara ya mahakama nchini kubuni kitengo maalum cha kukabiliana na wabakaji pamoja na kubuniwa sheria kali ili kuwalinda watoto wa kike kwani wengi wao huathiriki kisaikolojia.