Hali ya mshimshike ilishuhudiwa siku ya Jumatano mchana katika gereza la Jela Baridi eneo la King`orani Kaunti ya Mombasa baada ya wafungwa kujaribu kutoroka.
Mkuu wa gereza hilo Robert Basigwa alimweleza mwanahabari huyu kuwa wafungwa hao walikuwa wanataka kutoroka, lakini hakuna aliyefanikiwa kufanya hivyo baada ya polisi kuwakabili vilivyo.
Iliwalazimu maafisa wa polisi kufyatua risasi hewani kuzima jaribio la wafungwa hao ambao ni zaidi ya 500 kutoroka.
Basingwa aliongeza kuwa wafungwa hao walikuwa tayari wameshakata vyuma vya ndani na kupata nafasi ya kuanza kufika karibu na lango kuu.
Maafisa wa gereza waliligundua hilo kwa haraka ndipo wakaweka hali ya dharura kwa kutumia milio ya risasi kuwarudisha ndani.
Kwa sasa uchunguzi unaendelea ndani ya gereza hilo na watakaopatikana na hatia watahamishwa kutoka gereza hilo.
Hakuna aliye jehuriwa kwenye tukio hilo la siku ya Jumatano mchana.
Baadhi ya wafungwa waliowahi kufungwa ama kuzuiliwa katika rumande wamekuwa wakieleza kuwa gereza hilo limejaa kupita kiasi kutokana na watu kushikwa ovyo, idadi kubwa ya watu wanaofungwa kila siku katika mahakama kuu na mahakama ya serikali ya kaunti.