Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho, akosa mkutano wa Rais ambao uliandaliwa katika ikulu ndogo ya Sagana, huku naibu mwenyekiti wa magavana nchini Salim Mvurya, akiwakilisha eneo la Pwani japokuwa magavana 15 kutoka kaunti nyinginezo hawakuonekana kwenye mkutano huo.

Huenda tofauti za baina ya serikali ya Jubilee na gavana huyo kuhusiana na kufungwa kwa biashara ya familia pamoja tofauti za kisiasa kikawa chanzo cha kutohudhuria mkutano huo wa Rais.

Hata hivyo wakazi wa Mombasa wamesema kuwa naibu wa magavana nchini, ameweka wazi maono na mitazamo ya Wapwani baada ya kusisitiza umuhimu wa kuimarisha serikali za kaunti na kutengewa hela za kutosha ili kuziboresha zaidi na kufanikisha masuala lengwa kwa muda ufaao kabla ya muhula serikali za kwanza za ugatuzi kukamilika.

Akiongea siku ya Alhamisi kwenye ikulu ndogo ya Sagana katika kaunti ya Nyeri baada ya mkutano husika uliondandaliwa na Rais Uhuru Kenyatta, Mvurya alisema sharti serikali kuu iweke juhudi thabiti na kuupa mpango mzima wa ugatuzi nafasi pevu ya kutanda.

Kwenye mkutano huo Rais aliwahakikishia magavana kuwa serikali yake ipo tayari kushirikiana na serikali za kaunti ili kuboresha viwango vya maendeleo ambapo alitangaza kuwa serikali yake itapunguza matumizi ya fedha za usafiri kwa maafisaa wakuu serikalini kwa asili mia 40% na kuelekeza mgao wa fedha kutoka mikakati hiyo kupanua miradi ya serikali.

Mbali na Rais mkutano huo ulihudhuriwa na naibu wake Wiliam Ruto, mawaziri, pamoja na idadi ndogo ya magavana ambao waliongozwa na mwenyekiti wa magavana nchini Peter Munya.