Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amewasihi viongozi wa miungano ya walimu ya Knut na Kuppet kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakumbatia zoezi la usajili wa kura linalotarajiwa kuanza siku ya Jumatatu.
Hii ni kutokana na kwamba zoezi hilo litafanyika wakati ambapo masomo yatakuwa yakiendelea katika shule na vyuo vikuu kote nchini.
Joho ambaye pia ni naibu kinara wa chama cha ODM alisema kuwa viongozi hao pamoja na walimu wote kwa jumla wana ushawishi mkubwa kwa wanafunzi katika kuwahamasisha kuhusu zoezi hilo muhimu.
Katika hotuba yake wakati wa kikao na wanahabari kwenye hoteli ya Capital Hill mjini Nairobi siku ya Ijumaa, Joho alisema kuwa shule za upili pamoja na vyuo vikuu nchini vinafaa kuweka utaratibu unaofaa ili wanafunzi wapate muda wa kwenda kujiandikisha.
“Tunatoa wito kwa usimamizi wa shule pamoja na vyuo vyetu kuwapa wanafunzi muda wa kushiriki zoezi hili muhimu, na pia kuweka ratiba maalum ili waweze kupata nafasi hiyo,” alisema Joho.
Wakati uo huo gavana huyo aliwataka viongozi wote wa kisiasa humu nchini kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanafunzi hawanyimwi nafasi ya kushiriki zoezi hilo.
Licha ya kwamba haki ya kupiga kura ni ya kila Mkenya, kiongozi huyo alitaja vijana kama watu muhimu zaidi katika uchaguzi mkuu kwani ndio wengi zaidi nchini, na wengi wao wanapitakana katika shule za upili na vyuo vikuu.
Kauli ya Gavana Joho inakuja huku zoezi hilo la usajili likitarajiwa kuanza Jumatatu hii, tarehe Februari 15 hadi tarehe Machi 15 kote nchini.
“Nina hakika kwamba vijana wakijitokeza na kujiandikisha na pia wakipiga kura kwa wingi mwaka wa 2017 hatutasimama tena hapa tukilalamika kuibiwa kura,” alisema Joho.