Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa Mombasa Hassan Joho amewapongeza maskwota katika shamba la Waitiki kwa kuwa watulivu mpaka hatua ya mwisho ya kupewa hati miliki.

Akizungumza siku ya Jumamosi mjini Mombasa saa chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukamilisha shughuli hiyo ya kupeana hati miliki, Joho alisema kuwa wakaazi hao wamekuwa wavumilivu licha ya kuwa na mvutano hapo awali.

“Ningependa kuwashukuru wakaazi wa shamba hili kwa uvumilivu wenu hadi tamati. Nyinyi sasa ndio wamiliki wapya wa ardhi hii kutokana na ushirikiano wenu,” alisema Joho.

Wakati huo huo, Gavana Joho alisema kwamba serikali ya kaunti yake itashirikiana na Tume ya ardhi nchini NLC, pamoja na serikali kuu katika kusawazisha mambo ya malipo ya ada zitakazohitajika.

Maskwota wa Shamba la Waitikii walijawa na furaha kubwa pale Rais Kenyatta alipowasili katika eneo hilo siku ya Jumamosi kutoa hati miliki hizo.