Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amewataka vijana walioshikwa na maafisa wa polisi kinyume na sheria kuenda kortini na kuwashtaki dhidi ya dhuluma.
Gavana huyo amesema kuwa kamishna wa Kaunti hiyo Nelson Marwa amekuwa akiwaamrisha maafisa wa polisi kuwashika vijana wa kutoka mitaa mbalimbali ya kaunti hiyo na kuwatia mbaroni, ambapo wanawanyanyasa bila kupelekwa mahakamani na au wanapopelekwa mahakamani hawana hatia.
Akiongea siku ya Ijumaa katika eneo la Majengo katika eneo bunge la Mvita kwenye hafla ya uzinduzi wa barabara, Joho alisema kuwa si haki vijana kuwekewa makosa ambayo hayapo, na hata kupigwa na maafisa wa polisi, na kumtaka Marwa kuacha kuwahangaisha vijana ambao hawana hatia.
Alimshutumu kamishna huyo kwa kutoa picha za vijana ambao ni wadogo na kuwekewa mashtaka kuwa ni magaidi, na aliwataka maafisa wa polisi kukoma kuchukua hatua za kudhulumu vijana bila kuwa na ushahidi wa kutosha.
Aliwahimiza vijana ambao waliwahi kushikwa kinyume na sheria kuchukua hatua ya kisheria na kupata haki yao.
Matamshi hayo huenda yakaibua hisia mbalimbali, haswa kutoka kwa Marwa ambaye amekuwa akiendeleza vita dhidi ya vijana ambao wanajiunga na magenge ya kiuhalifu na wengine kuingia kwenye uharamia ambao umeshuhudia vijana wengi kutoka eneo la Pwani kuenda nchi ya Somalia kujiunga na Al Shabaab.