Gavana wa Mombasa Hassan Joho ametoa kauli yake kuhusu hatua ya idara ya polisi ya kumuondolea maafisa wake wa ulinzi mapema siku ya Alhamisi.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Joho alisema kuwa hatua hiyo ilichochewa kisiasa ikizingatiwa kwamba anatoka katika mrengo wa upinzani ambao amekuwa akiutetea vikali.
Gavana huyo aidha alisema anashangazwa na hatua ya kutohusishwa katika kufanya uamuzi kabla ya maafisa wake kuondolewa.
Wakati huo huo, pia alisisitiza kwamba atasalia katika muungano huo wa Cord licha ya misukosuko hiyo inayolenga kumtia hofu.
Inadaiwa kwamba masaibu yanayomkumba Gavana Joho yamesababishwa na ushindi wa chama cha ODM katika uchaguzi mdogo wa Malindi uliofanyika mapema wiki hii.
Maafisa saba wa usalama waliokuwa wakimlinda gavana huyo waliondolewa kazini siku ya Alhamisi kwa madai kwamba wameenda kupokea mafunzo zaidi.