Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho ameitaka serikali kuu kutowaganywa wakenya kwa kuwaahidi kuwapa ajira na badala yake kuwasajili vijana katika shirika la kitaifa la huduma kwa vijana nchini NYS.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Joho amesema kuwa kuwasajili vijana wa eneo la Pwani katika shirika hilo la NYS ni kuwahujumu na nafasi nzuri za kazi serikali inawapa vijana wengine.
Joho amesema kuwa iwapo serikali ina malengo ya kuajiri vijana na kuwawezesha kujikimu kimaisha, basi inafaa kubuni ajira katika mamlaka za serikali ikiwemo mamlaka ya bandari nchini, Mamlaka ya ndege nchini na idara zengine za serikali badala ya kuwahadaa wapwani.
“Kama serikali inajali maslahi ya vijana hususan wa Pwani, basi iwape ajira katika bandari ya Mombasa na katika mamlaka za umma na idara zingine za serikali wahudumie taifa hili katika nafsi kubwa kubwa, sio kutudanganya na nafasi za NYS na shirika liko na changamoto nyingi," alisema Joho.
Kauli ya Joho inajiri baada ya serikali kutangaza kurejesha upya usajili wa vijana kujiunga na shirika la kitaifa la huduma kwa vijana ili kuwawezesha vijana kujishughuli na miradi ya serikali.