Gavana wa Mombasa Hassan Joho amesema kuwa suluhu la matatizo ya shirika la feri nchini ni kuzindua daraja ya kuunganisha eneo la South Coast na kisiwani Mombasa, na kuwa daraja hilo litakuwa linalipiwa kama vile wateja wanapolipia kuvushwa katika kivuko cha feri eneo la Likoni ili kuimarisha mapato ya Kaunti ya Mombasa.
Akiongea siku ya Jumamosi kwenye maadhimisho ya siku kuu ya Jamhuri jijini Mombasa, Joho alisema kuwa kwa sasa sharti serikali ya kaunti ikae chini na kuhakikisha kuwa daraja hilo linatengenezwa haraka iwezekanavyo ili kuwaondolea wateja pamoja na wakazi wa eneo la Saouth Coast masaibu ya mara kwa ambayo wamekuwa wakikumbana nayo kwa muda mrefu sasa.
Joho pia amewataka viongozi wote wa kaunti kushikana mikono ili kusaidia kaunti hiyo kutatua matatizo yanayowakumba wakazi wote, siyo tu wa Mombasa, bali wa eneo zima la Pwani.
“Tutaweka juhudi za haraka kuona tunapata suluhu la feri kwa kujenga daraja ambalo litakuwa linatumiwa kama feri wateja wa kuvusha magari kwenye feri sharti walipie, hivyo sisi kama viongozi lazima tuje pamoja na kuona kuwa tunasuluhisha matatizo yote kwa njia ya pamoja,” alisema Joho.
Matamshi yake yaliungwa mkono na kamishna wa Kaunti ya Mombasa Bwana Nelson Marwa, ambaye alisema kuwa sharti maafisa wakuu wa shirika la feri kushirikiana na kupata suluhu la haraka ambapo pia alipongeza hatua ya Gavana Joho ya kuanza kutoa suluhu la kivuko hicho.