Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa kisiasa katika eneo la Pwani wamedai kubaguliwa na serikali kuu kwa kutotatua maswala tata ya mizozo ya ardhi na uimarishaji wa maendeleo.

Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa alisema kuwa kutokana na eneo la Pwani kutengwa na serikali kuu katika maswala ya kimaendeleo tangu uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2013 kamwe viongozi hao hawawezi kuunga mkono mrengo wa Jubilee.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Aisha amesema kuwa viongozi hao wataendelea kuunga mkono mrengo wa Cord kutokana na Menifesto yake jinsi inavyotetea maslahi ya wakaazi wa Pwani kwani tangu serikali ya Jubilee iingie madarakani hakuna mradi uliyofanyiwa wapwani.

Akionekana kuwarai wakaazi wa Pwani kuunga mkono mrengo wa Cord, Kiongozi huo amesema kuwa watahakikisha kuwa serikali ya Jubilee imeng’olewa madarakani kutokana na jinsi viongozi waliyomadarakani wanavyowabagua wakaazi wa Pwani.

"Sisi kama viongozi wa Pwani hatuoni kujiunga na serikali ya Jubilee kutokana na kuwa imetubagua wakaazi wa Pwani katika maswala ya kimaendeleo, ardhi zetu wanashindwa kutetea na kuacha mabwenyenye wakizinyakua hilo kamwe hatutakubali na kunawaomba wakaazi kuhakikisha kuwa wanaunga mkono Cord katika uchaguzi mkuu ujao," alisema Jumwa.

Kauli ya kiongozi huyo imeungwa mkono na mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Mombasa Mishi Mboko aliyedai kuwa kamwe viongozi hao hawatayumbishwa na serikali ya Jubilee.