Mshukiwa kwenye sakata ya wizi wa pesa kwenye shirika la huduma za vijana kwa taifa NYS, Josephine Kabura, alikosa kufika mbele ya tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi nchini, EACC.
Akimwakilisha mteja wake,wakili wa Kabura ameifahamisha tume ya EACC kwamba Kabura ni mgonjwa na ameomba kupewa muda wa hadi Jumanne ijayo kufika mbele ya EACC kutoa mwanga zaidi kuhusiana na hati ya kiapo aliyoiwasilisha mahakamani ambapo alimtaja waziri wa zamani wa ugatuzi, Anne Waiguru kama mshukiwa mkuu wa sakata hiyo ya ubadhirifu wa fedha kwenye sakata ya NYS.
Kwenye hati yake ya kiapo aliyoiwasilisha mahakamani mapema wiki hii, Kabura anadai kuwa Waiguru ni mmoja kati ya watu walionufaika na fedha hizo kwani alipanga njama ya kufanikisha wizi wa pesa hizo. Hata hivyo Waiguru amesisitiza kwamba hakuhusika vyovyote na ufisadi huo huku akitaja tuhuma hizo kama njama za kumuangamiza kisiasa.
Tume ya EACC iliwaagiza Waiguru na Kabura kufika mbele ya tume hiyo ili kuhojiwa kutoa mwangaza kuhusiana na sakata hio.