Share news tips with us here at Hivisasa

Kadhi mkuu wa Kenya Sheikh Shariff Muhdhar amesema uteuzi wa makadhi uliofanyika hivi majuzi haukufanywa na afisi yake bali tume ya huduma za mahakama.

Akizungumza na mwanahabri huyu siku ya Ijumaa, Kadhi alieleza kwamba alishirikishwa tu kushuhudia mahojiano na kuelekeza mahali palipohitajika ila hakuwa na uamuzi wa kadhi yupi kuajiriwa.

Aidha, aliitaka idara ya mahakama kuwa na uahangalifu zaidi siku za mbeleni wakati inapotangaza nafasi za kazi katika idara hiyo.

Wiki jana, viongozi wa baraza kuu la waislamu nchini (SUPKEM) walidai uteuzi huo haukuwa na uwazi.

Mwenyekiti wa baraza hilo ukanda wa Pwani Sheikh Muhdhar Khitamy alidai Kadhi mkuu pamoja na baraza la waislamu hawakuhusishwa kuwahoji makadhi hao.

Pia walidai kwamba sehemu zengine za nchi zilitengwa kwenye uteuzi huo.

Sheikh Khitamy alimtaka mwanasheria mkuu Githu Muigai kufutilia mbali orodha ya makadhi walioteuliwa na shughuli kuanza upya.