Kadinali John Njue amewahimiza Wakenya kujitokeza kwa wingi kwa minajili ya kushiriki ibaada takatifu ya misa itakayoongozwa na Baba mtakatifu Francisko siku ya Alhamisi.
Kupitia kwa barua iliyotumwa kwa parokia zote za jimbo kuu katoliki la Nairobi kadinali Njue aliwahimiza mapadri kuwahimiza Wakenya kutoka maeneo mbalimbali humu nchini kuungana na wakatoliki katika kumkaribisha baba mtakatifu.
“Wakenya wenye heri njema, bila ya kuzingatia dini zao au miaka wanaalikwa kwa misa itakayoongozwa na baba mtakatifu Francisko. Kutokana na hili, sisi sote tunahimizwa kufika jijini Nairobi kwa minaajili ya kuhudhuria misa hiyo,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Kadinali Njue pia alisema kuwa baba mtakatifu ameonyesha zama yake ya kukutana na Wakenya wengi iwezekanavyo wakati wa ziara yake hapa nchini, huku akiwahimiza wote wenye heri njema kujitokeza kwa minaajili ya kukutana naye.
Baba mtakatifu ataadhimisha ibaada takatifu ya misa katika uwanja wa chuo kikuu cha Nairobi, na pia atakutana na vijana katika uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani, Nairobi.
Pamoja na hayo, baba mtakatifu atakutana na viongzoi wa kanisa, wake kwa waume kutoka kote nchini katika shule ya St Mary’s Msongari.
Wakatoliki kutoka jimbo katoliki la Nakuru wanatarajiwa kuanza safari yao ya kuelekea jijini Nairobi baada ya ibaada takatifu ya misa itakayofanyika kwenye kanisa la Cathedral Church of Christ the King mwendo wa saa moja usiku, siku ya Jumatano.