Malumbano yanayoshuhudiwa kila uchao kuhusu aliye na mamlaka zaidi baina ya bunge la kitaifa na mahakama zinafaa kusitishwa ili kuona kwamba wananachi wanapata huduma bora hadi mashinani.
Haya ni kulingana na Mbunge wa Ruaraka Joseph Kajwang, aliyemwakilisha spika wa bunge la kitaifa nchini Justin Muturi katika kongamano la Muungano wa Jumuiya la mawakili wanahudumu katika bunge la Afrika wakati wa kujadili maswala muhimu yanayoisibu bunge hilo.
Akilihutubia kongamano hilo la siku mbili mjini Mombasa siku ya Alhamisi baada ya kulifungua rasmi, Kajwang alisema kwamba mawakili hao kutoka mataifa mbalimbali ya bara Afrika wanafaa kuibuka na vigezo muhimu vitakavyositisha mzozo wa kila uchao na kuyashauri mabunge na mahakama.
Wakati huo huo, ameitaka idara ya mahakama kusitisha mgogoro wa kuwaachisha kazi majaji wenye umri wa miaka 70 na kuyakabili maswala ya ufisadi katika idara hiyo kwa mujibu wa katiba ili kuwapa matumani ya kuhudumiwa vyema wakenya.
"Sioni kama kuna haja ya kujadili maswala ya kuachisha kazi majaji walio na umri wa zaidi ya miaka 70. Heri wajadili jinsi ya kusitisha kukithiri kwa ufisadi katika idara ya mahakama kwani mambo mengi yamebadilika katika idara hiyo kutokana na kashfa nyingi za ufisadi na kuharibu utekandakazi wa mahakama," alisema Kajwang.
Kwa upande wake, Karani wa bunge la senati Jeremiah Nyegenye alisema kwamba japo changamoto zipo baina ya idara ya mahakama na bunge la kitaifa, swala hilo litajadiliwa ili kuona kwamba mwongozo mwafaka wa mamlaka unapatika kwani mawakili hao wanahudumu kama washauri wa bunge la Afrika.
Kongamano hilo la siku mbili litakamilika na uchaguzi wa viongozi wa muungano wa jumuiya hiyo ya mawakili wa bunge la Afrika watakao hudumu kwa miaka miwili kuhakikisha wanayashauri vyema mabunge ya bara la Afrika.