Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameitaka tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kuthibitisha saini milioni moja na laki nne katika mfumo wa Okoa Kenya, ili wakazi wanufaike katika mipangilio ya chama pinzani cha Cord.
Akizungumza katika kongamano la kuhamasisha wakazi kujisajili kama wapiga kura katika eneo la Likoni, Kalonzo alisema kuwa iwapo wakazi watajisajili na kupiga kura siku ya uchaguzi, chama pinzani cha Cord kitaweza kunyakua ushindi na kuboresha maendeleo nchini.
Aidha, Kalonzo alisema kuwa katika baadhi ya mipangilio ya Okoa Kenya, chama cha Cord kitawalipia wakazi wa Likoni ada yote ya Shamba la Waitiki ili wakazi wapate hati miliki na kuendeleza maisha yao vyema.
Vilevile, Kalonzo amewataka vijana kulipigia kura chama cha Cord ili wanufaike na miundo msingi itakayowekwa na chama hicho, na kumaliza changamoto miongoni mwa vijana kama vile ukosefu wa ajira.
Kalonzo alisema kuwa hutua hiyo itawawezesha kujiepusha kutokana na kujiunga na makundi ya kigaidi yakiwemo MRC na Wakali Kwanza, miongoni mwa makundi mengine ya kigaidi.
Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar kwa upande wake aliwaonya wawakilishi wadi katika Kaunti ya Mombasa kutoitikia mwito wa ufisadi bila ya kuzingatia maslahi ya wakazi.
Kulingana na Seneta Omar, wawakilishi hao wameendelea kushinikiza mipangilio ya ufisadi katika Kaunti ya Mombasa na kusahau miradi inayolenga wakazi na kuendeleza ugatuzi.
Wakati huo huo, Mbunge wa Nyali Hezron Awiti aliunga mkono hatua ya Halmashauri ya Bandari nchini KPA kufunga biashara za familia ya Gavana Hassan Joho mwezi uliopita baada ya kunasa mali iliyokuwa imeingizwa nchini kinyume cha sheria, pamoja na madai ya kukwepa kulipa ushuru.
Aidha, Awiti amewataka wananchi kulipa ushuru ili kuboresha maendeleo nchini na maisha ya Wakenya kwa julma.