Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameitaka serikali kuu kuipa mamlaka zaidi tume ya ardhi nchini NLC ili iweze kushughulikia vilivyo maswala ya ardhi katika taifa hili.
Kalonzo alisema kuwa tume hiyo ina umuhimu mkubwa zaidi katika kushughulikia maswala ya ardhi nchini lakini imekosa kupewa uhuru wa kutekeleza majukumu yake.
Akiongea huko Likoni siku ya Jumapili, Kalonzo alisema kuwa tume hiyo imeshindwa kusuluisha changamoto ya ardhi katka ukanda wa Pwani kutokana na serikali kuingilia shughuli zake na hivyo kukosa nguvu dhabiti.
“Unyanyasi mkubwa hapa Kenya unapitia katika ardhi, na tunataka tume ya ardhi inayoongozwa na Mohamed Swaruzi kupewa mamlaka zaidi ili iweze kutatua mambo haya,” alisema Kalonzo.
Kiongozi huyo wa Cord pia aliwahimiza wakaazi wa Pwani kusimama kidete na kutetea haki yao kuhusu mashamba, akisema kuwa watu wenye mamlaka ya juu huchukua fursa hiyo na kunyakua mashamba ya Wapwani.
“Tume hiyo ikipewa nguvu itahakikisha kwamba hakuna mtu anayetoka eneo lingine na kuja kuwanyanyasa. Mnapaswa kufahamu kwamba ardhi ya Pwani ni ya watu wa Pwani,” aliongeza Kalonzo.
Aidha, Kalonzo alikosoa ziara ya Rais Uhuru Kenyatta katika eneo la Pwani mapema mwaka huu na kuitaja kama isiyokuwa na faida yoyote kwa Wapwani.
Kuhusu Shamba la Waitiki, Kalonzo aliirai serikali ya Kaunti ya Mombasa kujitolea na kusaidi maskwota wa shamba hilo kulipa pesa walizotozwa na serikali kuu.