Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amewataka viongozi wa kisiasa kutoka Pwani hasa wa chama cha Wiper kuwachunguza maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) kuhusu shughuli ya usajili wa wapiga kura katika eneo hilo.
Kalonzo alidai kuwa maafisa hao wameonekana kuwa na ushirikiano wa karibu na serikali na huenda wakachagia wizi wa kura wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Akihutubia wakaazi wa Likoni mjini Mombasa siku ya Jumapili, Kalonzo alisema kuwa kuna madai kuwa baadhi ya maafisa wa tume hiyo wameanza kuhama kituo kimoja hadi kingine baada ya masaa mawili, wakidai kuwa hatua hiyo inatokana na uchache wa vifaa vya kusajili wapiga kura.
Kalonzo alidai kuwa hatua hiyo ni njama tu ya kuzima mrengo wa Cord kisiasa, huku mrengo wa Jubilee ukijipatia umaarufu.
Kiongozi huyo alisema kuwa mrengo wa Cord hautakubali kuona wananchi wakinyanyaswa tena.
“Tafadhalini viongozi wenzangu chunguzeni hawa maafisa wa IEBC kuhusu shughuli hii ya usajili wa wapiga kura kwani kuna baadhi yao wanaopanga mikakati ya kuiba kura na kusaidia Jubilee kuingia uongozini tena,” alisema Kalonzo.
Kalonzo alikuwa ameandamana na viongozi wa kisiasa wa chama hicho katika eneo la Pwani ikiwemo Seneta wa Mombasa Hassan Omar, Mbunge wa Nyali Hezron Awiti pamoja na viongozi wengine wa chama hicho.