Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa kamati ya uchukuzi katika bunge la taifa Maina Kamanda amelitaka shirika la KFS kuimarisha uhusiano wa wafanyakazi na wakubwa wao, na kusema kuwa uchunguzi wa kina utafanywa katika shirika hilo kuhusiana na uagizaji wa vipuli ili kubaini iwapo utaratibu mwafaka unafuatwa wakati wa kununua vifaa hivyo.

Mwenyekiti huyo, ambaye alikuwa jijini Mombasa Ijumaa, alisema sharti uhusiano kati ya waajiriwa na wakubwa wao uwe mzuri ndio shirika lolote kuimarika na kutoa huduma pevu kwa wateja.

Kamanda alizuru kivuko cha Likoni na maafisa wengine kutoka idara ya uchukuzi ili kufanya ukaguzi kuhusiana na madai yamelikumba shirika hilo kwenye siku za hivi karibuni, huku kuu zaidi likitokea wiki jana ambapo feri tatu zilidaiwa na mamlaka hayo kuwa ziliharibika na kupeleka msongamano katika kivuko hicho. 

Mwenyekiti huyo alisema kuwa shirika hilo ni la serikali, na sharti lifanyiwe uchunguzi wa kutosha ili kubaini madai ambayo yamezuka dhidi ya bodi simamizi hususan mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Hassan Musa.

Ikumbukwe kuwa kulizuka lawama nzito kutoka kwa kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa wiki iliyopita shutuma ambazo alizielekeza kwa mkurugenzi wa shirika hilo ambapo kamishna huyo alimtaja Hassan kuwa kikwazo cha huduma mbovu zinazotolewa na KFS.

Ziara ya Kamanda imekuja siku tatu baada ya ile ya waziri wa uchukuzi John Mosonik kuwasili katika kivuko hicho cha Likoni, ambapo aliahidi kuharakisha uchunguzi kuhusiana na madai ya ufisadi ambapo tayari tume ya kupigana na ufisadi EACC inatarajiwa kuanza uchunguzi hivi karibuni dhidi ya KFS.