Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kamati ya leba katika Kaunti ya Mombasa ilifanya kikao maalum na usimamizi wa kiwanda cha kutengeza nguo cha EPZ siku ya Jumanne kujadili maswala mbalimbali yanayokumba kiwanda hicho.

Kamati hiyo ilitaka kupewa maelezo mwafaka kuhusu sababu ya kiwanda hicho kuwasimamisha kazi mamia ya wafanyikazi wake.

Akiongea wakati wa kikao hicho, afisa anayehusika na fedha katika kiwanda hicho Pankaj Mehta, alisema kuwa uamuzi huo uliafikiwa baada ya kiwanda hicho kukosa pesa zaidi za kuwalipa.

Hata hivyo, afisa huyo aliongeza kuwa wafanyikazi hao walikuwa wameajiriwa kwa kandarasi na kwamba muda wao wa kufanya kazi ulikuwa umekamilika, na hawangeweza kuwaajiri tena kutokana na changamoto hizo za kifedha.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kamati hiyo ya leba katika kaunti hiyo Tom Ogola alisema kuwa usimamizi wa kiwanda hicho unafaa kuendesha shughuli hiyo kwa kufuata sheria.

Ogola alisema kuwa kamati hiyo imeipa kiwanda hico makataa ya wiki moja kuwasilisha stakabadhi hizo kuonyesha kwamba muda wa kandarasi hiyo umekalika kihalali.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa wafanyikazi hao hawakutendewa haki na kwamba kamati hiyo ya bunge itahakikisha kwamba wanapata haki na kurejeshwa kazini.

“Tunaona kwamba EPZ hawataki kuwarudisha kazini lakini sisi kama kamati tunapendekeza kwamba hao wafanyikazi lazima warudishwe kazini kwa sababu wametolewa kwa njia ambayo sio haki,” alisema Ogola.

Takriban wafanyikazi 2,000 kutoka kampuni hiyo walipoteza kazi baada ya kandarasi yao kufutiliwa mbali na kiwanda hicho.