Kamati ya kuchunguza utumizi wa pesa za serikali katika Kaunti ya Kisii itatembelea miradi yote iliyofanywa katika wadi zote 45 za kaunti hiyo ili kubaini jinsi mawaziri wa kaunti hiyo walivyotumia pesa za serikali kufanya maendeleo.
Hii ni baada ya kamati hiyo kukamilisha uchunguzi wa kuwachunguza mawaziri wa kaunti hiyo jinsi walivyotumia pesa, jambo ambalo sasa litawalazimu kutembelea miradi ile mawaziri walieleza kufanya kabla ya kuandika ripoti kamili.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika bunge la Kaunti ya Kisii baada ya kukamilisha vikao vya kuwachunguza mawaziri hao, mwenyekiti wa kamati hiyo Ronald Onduso alisema watatembea katika wadi zote 45 za kaunti hiyo ili kuona maendeleo ambayo yamefanywa kupitia pesa hizo za serikali .
“Leo ilikuwa siku ya mwishio ya kuwachunguza mawaziri wetu 10 katika Kaunti ya Kisii jinsi walivyotumia pesa za serikali na waziri wa ardhi na miji Moses Onderi ndiye alikuwa wa mwisho,” alisema Onduso.
“Lakini kama kamati hatujaridhika jinsi pesa hizo zilitumika na tutaenda katika kila wadi ili kuhakikisha miradi ile tumeelezwa ilifanywa na pesa hizo," aliongeza Onduso.
Wakati huo huo, Onduso alisema wao kama kamati lazima watafuatilia kuona pesa za serikali zimetumika kwa njia ya halali kuhakikisha pesa zimetumika kunavyostahili.