Mahakama moja ya Nakuru siku ya Jumanne iliongeza kwa muda maagizo ya kutouzwa kwa mali ya kampuni ya maua ya Twiga Roses, kufuatia kodi inayodaiwa ya shilingi milioni 500.
Kampuni hiyo imeshtakiwa na kambi ya cray Fish iliyo Naivasha, baada ya kampuni hiyo kukosa kulipa kodi hiyo ya nyumba na faini iliyotozwa kwa wakati huo wote wa muda wa miaka mitano, baada ya kampuni hiyo kuingia kwenye mkataba na kambi hiyo wa kukodi ekari 150 za kipande cha ardhi kilicho kusini mwa ziwa la Naivasha.
Kesi hiyo ilijiri baada ya kampuni hiyo kuwekwa chini ya uangalizi (receivership) wa benki ya CFC Stanbic mnamo Februari mwaka wa 2014, baada ya kushindwa kulipa kiwango cha fedha ilichokuwa imetozwa hapo awali, hatua iliyopelekea wamiliki wa kipande hicho cha ardhi kudai mali ya kampuni hiyo kupitia kwa madalali (auctioneers).
Kutokana na hilo, madalali wa Nasioki Auctioneers walitangaza mnamo tarehe 5 Agosti mwaka huu kwamba mali ya kampuni hiyo ya maua itauzwa katika muda wa siku 14 iwapo fedha hizo hazitakuwa zimelipwa ili kupata kiwango hicho cha fedha.
Hata hivyo, jaji Maureen Odero wa mahakama ya Nakuru alitoa agizo la kuzuia hatua hiyo kuchukuliwa mnamo tarehe 18 Agosti, baada ya wamiliki wa Kambi ya Cray Fish kupitia kwa wakili wake kufika mahakamani na kupata maagizo ya kukusanya fedha ilizokuwa ikidai kampuni hiyo kupitia kwa madalali hao baada ya mali ya kampuni hiyo kuuzwa.
Kampuni hiyo ya maua ilihoji kuwa mali ambayo ilikuwa ikitakiwa kuuzwa ilikuwa chini ya kampuni ya CFC Stanbic, na kutokana na hilo, kambi ya Crayfish haikuwa na haki kisheria ya kukusanya fedha hizo baada ya mali hiyo kuuzwa.
Mameneja wa banki ya CFC, Kieran Day na Ian Small nao walihoji kuwa kampuni hiyo imelipa kodi yote kufikia sasa, na iwapo kuna kodi yoyote ambayo haikulipwa, ilikuwa inadaiwa kabla ya kampuni hiyo ya maua kuwekwa chini ya uangalizi wa benki ya CFC Stanbic
Kutokana na hilo, walikariri kwamba kambi ya Crayfsh haina haki ya kuuza mali yao.
Kesi hiyo sasa itasikizwa tarehe 18 Januari mwaka huu.