Kamishna wa Kaunti ya Kisii Chege Mwangi amewaomba wakaazi wa kaunti hiyo ambao walijiandikisha kupata vitambulisho vya kitaifa kufika katika afisi husika pamoja na kituo cha Huduma Center kuchukua vitambulisho vyao.
Kulingana na kamishna huyo, vitambulisho 12,000 bado havijachukuliwa na wenyewe, jambo ambalo alisema limesababisha msongamano mkubwa.
Akizungumza siku ya Alhamisi mjini Kisii, Mwangi alisema vitambulisho hivyo vimesalia katika afisi hizo kwa muda mrefu baada ya wakaazi kujiandikisha.
“Naomba wale wote waliojiandikisha kupata vitambulisho waje katika kituo cha Huduma Center mjini Kisii, au katika afisi yangu pamoja na zile za machifu kuchukua vitambulisho vyao,” alisema Mwangi.
Aliongeza, “Ningependa kuwahimiza wakazi kuchukua vitambulisho vyao ili waweze kushiriki katika zoezi la usajili wa wapiga kura kwa kuwa ni haki ya kila Mkenya ambaye ametimu miaka 18 kupata kitambulisho na kadi ya kura.”
Wakati huo huo, Mwangi aliomba wakaazi kuishi pamoja kwa upendo na amani.