Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Uasin-Gishu Abdi Hassan ametaka vijana, haswa Wa dini ya Kiislamu kujitahadhari na mitandao ya kijamii ambayo inatumiwa na magaidi.

Hassan alisema kuna magaidi ambao wanatumia mitandao ya kijamii kuendeleza ugaidi kwa kujificha katika dini ya Kiislamu.

Kulingana na Hassan, magaidi hao wanatumia mitandao hiyo kuendeleza uhasama wa kidini kwa kujifanya wafuasi wa dini ya Kiislamu.

“Nyinyi kama vijana wa Kiislam mjihadhari na matapeli ambao wanatumia mitandao ya kijamii kueneza jumbe za chuki na uhalifu kwa kujificha katika dini yetu,majangili hawa wanatumiwa na makundi ya kigaidi kugonganisha dini za humu nchini,” alisema.

Hassan alisema mara kwa mara vijana hunaswa na magaidi kupitia mitandao ya kijamii ili kuendeleza propaganda yao ya kugonganisha Wakenya kwa misingi ya kidini.

Aliitaka tume ya kitaifa ya uiano na utengamano NCIC kunoa makali yake dhidi ya watu ambao wanaendeleza uhasama miongoni mwa Wakenya kupitia kwa mitandao ya kijamii.

Hassan alikiri kwamba dini yao imetekwa nyara na magaidi hivyo basi vijana wapaswa kujihadhari na magaidi husika.

Wakati huo huo mwenyekiti wa baraza la maimam na wahubiri katika kaunti ya Uasin-Gishu sheikh Abubakar Bin amekashfu vikali swala la mashoga na wasagaji nchini humu.Alisema kuwa vitendo hivi ni vya kusikitisha sana haswa kwa vijana wetu.