Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amewaonya vikali wakazi wa kaunti hiyo dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao na kuwapa kichapo kikali washukiwa wa wizi.
Akihutubia wakazi wa kaunti hiyo mjini Nyamira siku ya Jumatano, Onunga alisema kuwa visa vya baadhi ya wananchi kuchukua sheria mikononi mwao kwa kuwachapa washukiwa wa uhalifu vinaendelea kuongezeka katika maeneo mengi kaunti ya Nyamira, hali iliyomlazimu kuwaonya wananchi dhidi ya mazoea ya kuchukua sheria mikononi mwao.
"Ni jambo la kushangaza kuwa visa vya wananchi kuchukua hatua na kuwachapa washukiwa wa uhalufu vinaendelea kushamiri katika maeneo mengi Nyamira, na sharti kila mmoja wetu aheshimu sheria kwa kuwa kuwachapa washukiwa wa wizi kwa nia ya kuua ni kinyume na sheri na kamwe hilo haliwezi kuruhusiwa," alionya Onunga.
Onunga aidha aliwasihi wananchi kuwasilisha washukiwa hao kwa maafisa wa polisi pindi tu wanapowashika badala yao kuchukua sheria mikononi mwao.
"Nawahimiza wananchi kuwashika na kisha kuwawasilisha washukiwa wa aina hiyo kwa maafisa wa polisi ili hatua kuchukuliwa dhidi yao badala ya kuchukua sheria mikononi mwenu kwa kuwachapa washukiwa kwa nia ya kuwaua," alisihi Onunga.
Haya yanajiri baada ya washukiwa wawili wa wizi wa kimabavu kupokea matibabu kwenye hospitali kuu ya Kisii baada ya wakazi wa Nyamira mjini kuwapa kichapo cha mbwa mapema wiki jana.