Kamishna wa Kaunti ya Nyamira amewaonya wanaowahangaisha wananchi.
Haya yanajiri kufuatia visa vya utovu wa usalama kuendelea kuripotiwa katika maeneo mengi katika kaunti hiyo, hasa msimu huu wa Krismasi.
Akihutubia wanahabari afisini mwake siku ya Jumatatu, Kamishna Josephine Onunga alisema kuwa afisi yake imeweka mikakati kuhakikisha kuwa yeyote atakaye naswa akijihusisha na visa vya uhalifu atachukuliwa hatua kali.
"Afisi yangu imeweka mikakati kuhakikisha kuwa visa vya uhalifu vinakabiliwa vikali. Yeyote atakaye patikana akijihusisha na uhalifu atachukuliwa hatua kali za kisheria na kamwe hatutosita kukabiliana na uhalifu hadi pale visa hivyo vitakavyo thibitiwa," alisema Onunga.
Onunga alisema kuwa maafisa wa polisi watashika doria kote Nyamira ili kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa, akiongeza kuwa tayari maafisa walioko kwenye likizo wamelazimika kurejea kazini ili kuhakikisha kuwa usalama wa wananchi unadumishwa.
"Maafisa wa polisi watakuwa wakishika doria katika maeneo ambayo yamekuwa yakiripoti visa vingi vya uhalifu, hasaa katika maeneo ya Magwagwa, Nyamusi na Keroka. Tayari maafisa walioenda kwenye likizo wamelazimika kurejea kazini ili kuhakikisha kuwa hilo linaafikiwa," alisema Onunga.