Maafisa wa polisi kaunti ya Kilifi wametoa onyo kali dhidi ya wanaofadhili kundi hili.
Akiwahutubia wanahabari katika ofisi yake siku ya Jumanne kamishna wa kaunti ya Kilifi Joseph Keter ametangaza kuwa wanawake wanatumika katika zoezi la kuwaandikisha upya wanachama wapya.
"Kulingana na taarifa tulionayo, kuna kadi zinazouzwa na kusambazwa kwa wanachama wapwa kwa shilingi 100. Kadi hizo zinawataka wanachama kuonyesha uzalendo wao na wamechukua fursa hii kukoroga maafisa wa polisi, lakini tutawatafuta na kuwapata," alisema Keter.
Haya yanajiri baada ya taarifa kuwa MRC inaajiri vijana eneo la Mombasa na viunga vyake ili kulemaza usalama Pwani.
Aidha viongozi wa vuguvugu hilo wameshtumu kauli hiyo ya maafisa wa polisi na wanasema polisi inatumia kundi hilo kuwapiga vita na kuwamaliza kisiasa baadhi ya watu eneo la Mombasa.
"MRC haijahusika katika vurugu wala mauwaji yoyote, asiwadanganye mtu, sisi tunapigania haki kwa kueneza amani," alisema mmoja wa viongozi.
Onyo hili linajiri siku kadhaa baada ya wanachama 42 wa vuguvugu hilo kukamatwa katika eneo la Tiwi, Pwani Kusini na imebainika kuwa 12 walikuwa ni wazaliwa wa kaunti ya Kilifi.