Kufuatia visa vya watu kuuliwa katika Kaunti ya Nyamira na watu wasiojulikana kamishna wa kaunti hiyo Josphine Onunga amejitokeza kuwaonya vikali wahusika.
Akihutubu kwenye mkutano wa pamoja wa kufungua mwaka na washikadau wa masuala ya usalama kwenye mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Jumamosi, Onunga alisema maafisa wa polisi wataimarisha oparesheni zao hasa majira ya usiku ili kuwakabili wahalifu, huku akihoji kuwa magari na pikipiki zinazosafirisha watu usiku yatakuwa yakifanyiwa pekisheni.
"Haiwezekani kuwa mwezi haupiti kabla ya kusikia ripoti kwamba kuna watu wameuliwa eneo fulani, na ndio maana tumeweka mikakati ya kuhakikisha maafisa wa polisi wanafanya oparesheni kali usiku na hata pia kupiga pekisheni magari na pikipiki zinazosafirisha watu usiku ili kuthibiti visa hivi vya uhalifu," alisema Onunga.
Akizungumzia suala la kuthibiti usalama vijijini, Onunga alihimiza wakazi wa kaunti hiyo kupiga ripoti kwa maafisa wa usalama iwapo kuna watu wanao washuku kuwa tishio kwa usalama wao.
"Tunaweza tu kufanikiwa kuthibiti hali ya usalama vijijini iwapo tu wananchi watashirikiana nasi kiukamilifu kwa kuripoti watu wanao washuku kuwa tishio la usalama wao kwa maafisa wa polisi," aliongezea Onunga.