Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga amewahimiza machifu kutumia vizuri pikipiki walizopokezwa na serikali ya kitaifa kwa minajili ya kuimarisha usalama katika maeneo yao ya utawala.
Akihutubia wakazi wa Nyamaiya siku ya Jumapili, kamishna Onunga alisema pikipiki hizo zilipeanwa maafisa hao wa utawala kwa minajili ya kuimarisha usalama wa kaunti hiyo, huku akiwaonya vikali machifu dhidi ya kutumia pikipiki hizo kwa manufaa yao yakibinafsi.
“Kwa sababu ya uaminufu mkubwa tulio nao kwa machifu ndio maana tukawapa pikipiki ili waimarishe usalama wa wananchi katika maeneo yao ya utawala, na sita sita kuwachukulia hatua kali wale watakaopatikana wakizitumia kwa manufaa yao ya kibinafsi," alionya Onunga.
Onunga aidha aliwahimiza machifu kutumia pikipiki hizo kutembelea maeneo yao ya utawala il kuwahudumia wananchi, huku akisema kuwa mazoea ya kufanyia mikutano katika eneo moja husababibisha wananchi wengi kutohudhuria mikutano husika kwa sababu kwamba baadhi yao hawawezi mudu kufika katika maeneo hayo.
“Nahitaji kuona machifu wakifanya mikutano katika sehemu mbalimbali za maeneo yao ya utawala na wala sio kuketi tu afisini kwa maana sharti machifu wahakikishe kwamba maeneo yao ya utawala yako salama na itakuwa jambo zuri iwapo watakumbatia wazo la kufanya," aliongezea Onunga.