Kampuni ya maji ya mji wa Naivasha imesema kuwa imeanzisha mfumo wa kuwazadi wakazi ambao watakuwa wakiripoti matukio ya kuharibiwa kwa mifereji yake.
Hii ni kutokana na ongezeko la uharibifu wa laini za kupitishia maji huku mifereji hiyo ikiibiwa tukio ambalo linawafanya wakazi hao kukosa maji.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Joseph Theuri alisema kuwa wale watakaoripoti pindi tu wanapoona uharibifu huo ukifanywa watazawadiwa na washukiwa kutiwa mbaroni.
Akizungumza Jumamosi, Theuri alisema kuwa wameanzisha pia msako wa wale wote waliounganisha laini za mifereji kwenye ploti zao bila ya kuzingatia sheria.
“Tutahakikisha kuwa wote waliounganishiwa mifereji katika ploti na ambao hawalipi ada za maji wanachukuliwa hatua,” Theuri alisema.
Aidha mkuu huyo amewataka wale wote walio na madeni ya maji kulipa ili kuweza kuendeleza huduma bila ya kusitisha ili wote waweze kupata bidhaa hiyo muhimu.