Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mzozo baina ya wakazi wa eneo la Miritini na kampuni ya ujenzi wa reli mpya ya SGR unatarajiwa kupata suluhu baada ya makundi yote mawili kukubaliana kufanya kikao cha pamoja.

Kikao hicho kilichoratibiwa kufanyanwa siku ya Ijumaa kinatarajiwa kujadili kwa kina kuhusu swala la fidia ambalo wakazi hao wamekuwa wakililia kwa muda mrefu.

Kikao hicho kinakuja siku chache baada ya mzozano kuzuka baina ya wakazi hao na kampuni hiyo, wakati ilipotaka kubomoaa eneo la makaburi kwa nguvu huku wakazi hao wakiapa kuzuia umobozi huo.

Kulingana na wakaazi hao ni kwamba kampuni hiyo ilitoa ahadi ya kutoa fidia ya shilingi elfu 50 kwa kila kaburi katika eneo hilo, lakini baadae mpango huo ukabadilishwa na ubomozi ukaendelea.

“Tulikubaliana vizuri wakatupatia stakabadhi na tukawa tunangoja pesa lakini baadae tukaanza kuona ujenzi ukiendelea bila kushauriwa,” alisema Charo Kosi, mmoja wa wakazi hao.

Hata hivyo, maafisa wanaoshughulika na ujenzi huo wamelaumiwa kwa kuendeleza ubomozi bila kufuata sheria huku wakidaiwa kuharibu maeneo muhimu.

Wenyeji walisema kuwa viongozi wa eneo hilo hawajafanya lolote kuhakikisha kuwa wanapata haki, huku baadhi yao wakisusia mikutano inayoitishwa na wakazi.

“Wakati wa mikutano hatumuoni kiongozi wa mtaa wala chifu wetu na tunajiuliza kama kweli wanajali matatizo tunayopitia,” alisema mkaazi mmoja.

Shirika la kutetea haki za kibinadamu Muhuri limethibitisha kuhudhuria kikao hicho ambapo wanatarajiwa kufuatilia kwa makini mzozo huo na kutoa mwelekeo unaofaa.