Kampuni za Autoport na Portside zilizofungwa na Halmashauri ya ukusanyaji ushuri nchini KRA kwa ushirikiano na Halmashauri ya Bandari ya Mombasa KPA, kwa madai ya kutolipa kodi na kuingiza bidhaa ghushi nchini sasa zimepewa idhini ya kuzirejelea shughuli zake za kawaidi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza na wanahabari katika Bandari ya Mombasa siku ya Alhamisi, mkuu wa polisi katika Halmashauri hiyo, Zacheus Ng'eno, alisema kuwa kampuni hizo zimeruhusiwa kuhudumu tena ila zimepigwa marufuku kuyaingiza makasha mengine mapya hadi uchuguzi unaofanywa na maafisa wa KRA utakapo kamilika.

Ng'eno alisema kuwa kuingizwa kwa makasha mengine mapya, kutahitilafiana na uchunguzi unaoendelea.

Kwa juma moja sasa, kumeshuhudiwa mvutano baina ya maafisa wa KRA na usimamizi wa kampuni hizo mbili, zinazodaiwa kumilikiwa na familia ya Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho.

Siku ya Jumatano KRA iliongoza shughuli ya kuziaribu bidhaa ghushi zinazodaiwa kuingizwa nchini kupitia kampuni hizo.

Aidha, siku ya Jumanne,maafisa wa polisi waliojiami kwa bunduki walizingira kampuni hizo na kuwaagiza wafanyikazi kuondoka mara moja, licha ya wakurugenzi wa kampuni hizo kupata kibali cha mahakama kilichowapa idhini ya kuhudumu.

Kufunguliwa kwa kampuni hizo kutaleta afueni kwa wafanyikazi zaidi ya 1,200 ambao wako katika hatari ya kupoteza ajira iwapo kampuni hizo zitafungwa.