Katibu wa hazina ya maendeleo katika eneo bunge la Bahati Colins Oduor ametoa wito kwa vijana wa eneo bunge hilo kuhakikisha wanajitokeza ili wapate kunufaika.
Akizungumza afisini mwake Jumatatu, Oduor, ambaye pia anasimamia maswala ya vijana eneo la Bahati anasema kuwa ni jambo la kusikitisha kwa vijana kutojitokeza katika mambo makuu ya maendeleo.
"Vijana wanasalia nyuma kwa sababu hawana ari ya kupata habari muhimu kuhusu maendeleo, na nawaomba wamakinike sasa," alisema Oduor.
Wakati huo huo amedokeza kuwa Afisi ya mbunge Kimani Ngunjiri wa eneo bunge hilo ameanzisha mpango wa kuhakikisha vijana wanapata mafunzo na leseni za kuendesha magari au pikipiki.
Kulingana naye, vijana wengi wanahangaishwa na polisi kwa kukosa leseni, swala ambalo anasema hivi karibuni litakuwa limezikwa katika kaburi la sahau.