Utawala wa kaunti ya Uasin Gishu utachukua usimamamizi wa uwanja ndege mdogo wa Eldoret ili kuboresha utunzi na usimamizi wa uwanja huo.
Gavana wa kaunti hiyo Jackson Mandago amesema hatua hiyo ni mojawapo wa mbinu ambazo utawala huo unatumia ili kuboresha sekta ya utalii katika kaunti za North-Rift.
Mandago alisema sheria ya ugatuzi inaruhusu utawala wa kaunti kupewa usimamizi wa uwanja huo. Pia alisema tayari mazungumzo kati ya malaka ya ndege nchini KAA na utawala huo yanendelea.
“Tunazungumza na wadau wengine ili kuona kwamba mipango hii imefaulu, sheria ya ugatuzi inaturuhusu kutwaa usimamizi huo kwa ushirikiano na wadau wengine,” alisema Mandago.
Gavana Mandago alisema kuna haja ya kuhamasisha wananchi mashinani kuhusu umuhimu wa kukumbatia usafiri kupitia kwa ndege ili kurahisisha na kuboresha shughuli za biashara.
Mandago alisema utawala wake kwa ushirikiano na kaunti nyingine za North-Rift unapanga kuwa na viwanja vya ndege katika kila kaunti ili kuwe na safari za ndege kati ya kaunti hizo.
“Kuna haja ya wakulima na wanabiashara wengine kutoka North-Rift kuhamasishwa kuhusu umuhimu kukumbatia safari za ndege kinyume na kasumba potovu kwamba safari za ndege ni za watu matajiri tu,” alisema Mandago.