Share news tips with us here at Hivisasa

Waziri wa Kilimo katika Kaunti ya Kisii Vincent Sagwe amesema serikali ya kaunti hiyo itawekeza katika ukulima wa kisasa kwa kila wadi ili kuongeza mazao.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Kisii, waziri Sagwe alisema kubwa ya wakulima wa kaunti hiyo wamekuwa wakipata hasara kubwa wanapofanya kilimo kufuatia kuathirika kwa mimea wanaopanda kutokana na magonjwa mbalimbali, jambo ambalo lilipelekea serikali kufikiria kilimo cha kisasa ili kutoa usaidizi.

Kulingana na Sagwe, serikali ya kaunti imeweka mikakati ya kuwekeza katika Greenhouse kwa kila wadi ili kilimo cha kisasa kuanzishwa ambacho kinatarajiwa kutoa msaada mkubwa kwa wakulima.

“Serikali ya kaunti inahitaji kukomesha hasara ambazo zimewaathiri wakulima wetu maana wanapofanya kilimo cha Nyanya, sukuma wiki huathiriwa na magonjwa mbalimbali, sasa tutaweka Greenhouse kila wadi ili kilimo cha kisasa kianze kufanya kazi,” alisema Sagwe.

Aidha, Sagwe alisema hivi karibuni maafisa wa kilimo katika kaunti ya Kisii watatembea katika kila wadi na kutoa mafunzo bila malipo jinsi wakulima watakuwa wakitumia Greenhouse kufanya kilimo cha kisasa.

Sagwe pia aliomba wakazi wa kaunti hiyo kujaribu kila wawezalo kuhakikisha kila mtu amekumbatia kilimo cha kisasa ili kujiendeleza.

“Naomba kila mkazi wa kaunti hii kuanzisha kilimo cha kisasa ili kupata faida nyingi. Serikali imepanga jinsi itatoa mafunzo bila malipo kwa wakazi kila wadi jinsi ya kufanya kilimo cha kisasa,” aliongeza Sagwe.